Kapingaz Blog

Friday, August 17, 2018

Waziri Dk. Kigwangalla kuruhusiwa muda wowote MOI.....Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Amtembelea tena

Na Andrew Chale, Dar
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI,  hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.


Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8,2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15,2018 katika wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu  aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani  huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini hapo.
Waziri Mkuu Atoa Maagizo Mazito kwa Wakuu wa Wilaya Nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini washirikiane na Madiwani katika halmashauri zao wafanye tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema licha ya tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kiduchu, jambo linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Nzega, Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba Serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.

Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Nzega uliamua kupitia upya mkataba wa mradi huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi, hivyo ilianzisha mpango wa maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati waliokuwa wakiwatoza wafanyabiashara zaidi ya sh 150,000 kwa mwenzi na kuilipa halmashauri sh. 30,000 kwa mwezi.

Pia ilibaini kwamba baadhi ya wamiliki wa awali wa vibanda waliviuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya kuishirikisha halmashauri na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara waendelee kuwa wapangaji kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka mgogoro wa umiliki wa vibanda hivyo.

Waziri Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo huwa haiishi kwa wakati katika maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo vinamilikiwa na Wakuu wa Idara, Madiwani na baadhi ya watumishi katika hailashauri husika, jambo linalozikosesha halmashauri mapato. “Wakuu wa wilaya shughulikieni hili,”.

Pia, Waziri Mkuu amezishauri halmashauri zinazomiliki vibanda vya biashara hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie leseni za biasahara zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na wamiliki wake ili kuondoa uwepo wa mtu wa kati.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wanaomiliki vinanda vya biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za umiliki wao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya kujadili namna bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri na wilaya wawahamasishe wananchi kwenye maeneo yao juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), hivyo watakuwa wamejihakikishia upatikanaji wa huduma za afya bure kwao na familia zao.

Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Agrey Mwanri kwa jitihada kubwa za kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya kupitia CHF, ambapo kwa mkoa huo wanachama wa mfuko huo wanaweza kutibiwa kwenye hospitali zote za Serikali tofauti na maeneo mengine ambayo huduma hiyo inaishia kwenye hospitali za wilaya tu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.

Katibu Mkuu CCM Naye Kajitosa Sakata la Ubalozi wa Marekani Kudai Uchaguzi wa Marudio Haukuwa Huru na wa Haki

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameitaka Marekani na taasisi za kimataifa kuheshimu uhuru wa Tanzania.

Amesema kauli iliyotolewa na Marekani kuhusu uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika Agosti 12, mwaka huu katika maeneo mbalimbali nchini, inagusa maeneo mengi na ni matarajio yake kwamba taasisi zote za nchi zinazohusika zitazingatia madukuduku yao.

Kauli hiyo ya Dk. Bashiru imekuja siku mbili baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa tamko kuhusiana na uchaguzi huo ambapo ilisema uligubikwa na vurugu na pia haukufuata sheria.

“Nimeisoma na nimeielewa, sisi kama chama, tunazingatia zaidi uhuru wa kitaifa kwamba taifa hili ni taifa huru na CCM kina dhamana ya kusimamia uhuru wa kitaifa.

“Ninachojua mimi chaguzi zote zimefanywa kwa msingi wa sheria na matarajio yangu ni kwamba Marekani na taasisi nyingine za kimataifa, zitaheshimu uhuru wa taifa letu,” amesema Dk. Bashiru akihojiwa Kituo cha Deustche Welle cha Ujerumani.

Madiwani Wengine Wawili CHADEMA Wajiuzulu na Kuhamia CCM Leo

Madiwani wawili wa Chadema mkoani Kilimanjaro  wamejivua uanachama na kujiunga na CCM.

Waliohama chama hicho leo Agosti 17 ni aliyekuwa diwani wa kata ya Romu wilayani Hai, Shilyimaufoo Kimaro na diwani wa kata ya Vumari, Wilayani Same, John Msofe.

Akizungumzia kuondoka kwa madiwani hao Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanajro,Basil Lema amesema ni kweli madiwani hao wameondoka kwa kile wanachodai wao ni kuunga mkono juhudi za Rais.

Lema amesema kuwa anajua madiwani hao wanahama chama hicho kutokana na baadhi yao kutishiwa uhai na usalama wa maisha yao na wengine wanaondoka kwa sababu ya madeni waliyonayo au maslahi yao binafsi.

“Madiwani wanaobaki wabaki na wale wanaoondoka waondoke lakini tunajua wanaondoka kwa sababu ya vitisho wanavyopata na wengine wanaondoka kutokana na madeni walionayo wakijifanya wanaunga mkono jitihada za Rais,”amesema.

Madiwani Wengine Wawili CHADEMA Wajiuzulu na Kuhamia CCM Leo

Madiwani wawili wa Chadema mkoani Kilimanjaro  wamejivua uanachama na kujiunga na CCM.

Waliohama chama hicho leo Agosti 17 ni aliyekuwa diwani wa kata ya Romu wilayani Hai, Shilyimaufoo Kimaro na diwani wa kata ya Vumari, Wilayani Same, John Msofe.

Akizungumzia kuondoka kwa madiwani hao Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanajro,Basil Lema amesema ni kweli madiwani hao wameondoka kwa kile wanachodai wao ni kuunga mkono juhudi za Rais.

Lema amesema kuwa anajua madiwani hao wanahama chama hicho kutokana na baadhi yao kutishiwa uhai na usalama wa maisha yao na wengine wanaondoka kwa sababu ya madeni waliyonayo au maslahi yao binafsi.

“Madiwani wanaobaki wabaki na wale wanaoondoka waondoke lakini tunajua wanaondoka kwa sababu ya vitisho wanavyopata na wengine wanaondoka kutokana na madeni walionayo wakijifanya wanaunga mkono jitihada za Rais,”amesema.

Nape Nnauye Atoa Kauli Kuhusu Wabunge na Madiwani Wanaohama Vyama

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema ipo haja ya kupitiwa upya kwa sheria inayosimamia thamani ya kura hasa katika kipindi hiki cha wabunge na madiwani kuhama vyama vyao.

Nape amesema kuwa  ni vyema kukawa na sheria ambayo itampa mamlaka mbunge au diwani anayehama chama baada ya uchaguzi, aendelee kuwa na nafasi hizo katika chama anachokwenda ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika chaguzi ndogo kwenye maeneo ambayo mbunge au diwani amehamia chama kingine.

Ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ofisi ndogo za Bunge visiwani Zanzibar, katika mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na wajumbe wa tume ya utumishi wa Bunge ambapo amesema pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wanasiasa kuhama, wapigakura wanatakiwa kupewa thamani yao kwa kuwa wakati wa uchaguzi wao ndio uhitajika kupiga kura kuchagua wawakilishi wao.

"Siwezi kupingana na Katiba kuhusu hamahama za wanasiasa lakini ni vyema thamani ya wapiga kura ikatambulika vyema, bado thamani ya mpiga kura inapaswa kuenziwa,” amesema Nape.

Wakati hayo yakijiri Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally anatarajiwa kufanya  ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humo kuanzia leo  Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.

Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.

IGP Sirro: Tuko Vizuri, Moto Wetu ni Mkali kwa Sasa

Na Jeshi la Polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ametoa onyo kali kwa majambazi na wahalifu wengine hususani wanaotumia silaha za moto kuacha mara moja kabla ya kukutana na moto mkali wa Jeshi la Polisi ambapo pia ametoa wito kwa wazazi kuwakanya watoto wao kujihusisha na vitendo hivyo.

IGP Sirro ameyasema hayo wakati akizungumza na Wakazi wa Mto wa Mbu Tarafa ya Manyara Wilayani Monduli Mkoani Arusha wakati wa Ziara yake mkoani humo yenye lengo la kubaini changamoto za kiuhalifu na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema hivi sasa ujambazi wa kutumia silaha umepungua kwa kiasi kikubwa na baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza yanaendelea kudhibitiwa na Jeshi la Polisi.

“Nawasihi wanaofikiria kuendelea kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo vya utumiaji wa silaha na kuua watu waache mara moja kwa kuwa wakikutana na moto wa Jeshi la Polisi wasije wakajilaumu mana kwa sasa moto wetu ni mkali hivyo nawashauri wazazi wakanye watoto wao” Alisema Sirro.

Aidha amewataka Wakazi wa Mto wa mbu Wilayani Monduli kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa usalama umeimarishwa katika kupambana na wahalifu waliokuwa wakifanya vitendo vya kuwaua watu hususani wanawake ambapo katika kipindi cha hivi karibuni kuliripotiwa matukio kadhaa ambayo yalileta wasiwasi katika eneo hilo muhimu kwa utalii.

Amewataka Viongozi wa Vijiji na Kata kuhakikisha kuwa suala zima la ulinzi na usalama linatiliwa mkazo ili kuhakikisha hakuna mhalifu katika maeneo yao na wageni wanapoingia wachukue taarifa zao mapema.

Kwa Upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mto wa Mbu Bi. Kuluthum Hassan alisema Wahalifu wanaouza bangi, pombe ya gongo na dawa za kulevya wanaendelea kuwafichua ili wafikishwe katika vyombo vya dola na hivi sasa wanaendelea na mipango ya ujenzi wa kituo kikubwa cha Polisi kitakachoendana na hadhi ya eneo hilo.

Nao wananchi mbalilmbali wa Mto wa mbu wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanakuwa salama wakati wote hususani kipindi hiki cha watalii wengi katika maeneo hayo na wameahidi kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi ili kuboresha usalama katika eneo hilo.