Kapingaz Blog

Tuesday, August 9, 2011

MNYAMA WA AJABU ATOKEA DUNIANI

Hapa Chupacabra akiwa anamlia taimingi Mbuzi ili amnyonye damu

UVUMI umeenea nchi za bara la Amerika kwamba kuna mnyama aitwaye Chupacabra (inatamkwa ‘Chupakabra’) ambaye hushambulia na kunywa damu ya mifugo hususan mbuzi huku wengine wakidai ni binadamu wengine wakisema ni mnyama.

Mnyama huyo wa ajabu amedaiwa kuonekana huko Puerto Rico kwa mara ya kwanza mwezi Machi mwaka 1995, Mexico, Marekani, na nchi za kusini mwa bara hilo.

Kiumbe huyo aliyechenga akili za watu wa kawaida na wataalam ameripotiwa pia kuonekana Russia na Ufilipino (The Philippines) akiwa na umbo la dubu mdogo, shingo ndefu na mkia mrefu.

Wataalam wa viumbe na wanyama pori wanamwelezea mnyama huyo kama “wa sasa” yaani hakuwepo huko nyuma.
Watu wa kawaida wanadai mnyama huyo yupo, lakini wataalam kwa ujumla wanasema hayupo!
Mnamo Julai 2010, aliuawa mnyama aliyedhaniwa kuwa Chupacabra huko Puerto Rico, lakini baadaye akagundulika kuwa ni mbweha aliyekuwa ameugua ugonjwa wa ngozi.

Hivyo wataalam wakasema kinachodaiwa kuwa ni Chupacabra ni mbweha waliokumbwa na ugonjwa huo.
Chupacabra amepewa jina hilo la Kihispania ambalo linatokana na maneno “chupar” linalomaanisha “kunyonya”, na “cabra” likimaanisha “mbuzi”.

Tangu 1995 idadi kadhaa ya mifugo, hususan mbuzi na kondoo, wamegunduliwa wamekufa wakiwa na majeraha kifuani na wakiwa wamenyonywa damu yote miilini mwao, jambo ambalo linaaminika ni mashambulizi ya Chupacabra.
Habari ndiyo hiyo! Inatukumbusha uvumi kama huo hapa nyumbani uliohusu Popobawa.

0 comments: