Kapingaz Blog

Friday, February 3, 2017

Rais Dkt Magufuli aeleza kusikitishwa kwake na namna mahakama inavyoshughulikia kesi za ukwepaji kodi.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na namna Mahakama inavyoshughulikia kesi zinazohusiana na ukwepaji wa kodi na ametoa wito kwa mahakama na wadau wake kujipanga kukabiliana na dosari hiyo inayorudisha nyuma juhudi za maendeleo ya nchi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Februari, 2017 katika sherehe za uzinduzi wa mwaka wa Mahakama (Siku ya Sheria) zilizofanyika katika uwanja wa Mahakama uliopo Mtaa wa Chimala, Kivukoni Jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2016 Serikali haijalipwa kiasi cha Shilingi Trilioni 7.5 licha ya kushinda kesi za ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa mbalimbali.

Dkt. Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa kazi kubwa inayofanywa kuleta mabadiliko na uboreshaji wa huduma na miundombinu na ametaka kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Umuhimu wa utoaji wa haki kwa wakati kuwezesha ukuaji wa uchumi” itekelezwe vizuri kwa kutanguliza maslai ya Taifa ikiwemo kuhakikisha wanaopatikana na hatia ya kukwepa kodi wanalipa.

“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi.

“Sasa tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa kiasi gani kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mahakama wajipange kwa pamoja ili kushughulikia ipasavyo mashauri mbalimbali na kuondokana na migongano ambayo imekuwa ikidhohofisha ufanisi wa shughuli za kimahakama.

Pia Dkt. Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la ufinyu wa bajeti na maslai ya wafanyakazi wa Mahakama wakiwemo Majaji.

Pamoja na kumpongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Mahakama, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma amesema katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, mwaka 2016 jumla ya mashauri 279,331 yamesikilizwa sawa na asilimia 101 ya matarajio ya kusikiliza mashauri 276,147, Mahakama imefanikiwa kumaliza kesi 248 kati ya kesi 249 za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilizohusisha Ubunge na Udiwani na pia Mahakama Kuu imefanikiwa kuanzisha Divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi (Mahakama ya Mafisadi)

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. John Kijazi, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Leons Wambali, Majaji wa Mahakama Kuu, Mawakili, Viongozi wa Dini na Siasa na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

02 Februari, 2017

0 comments: