Kapingaz Blog

Thursday, February 9, 2017

TAHADHARI KWA WAMILIKI WA ARDHI WENYE MADENI YA PANGO LA ARDHI


AAA
Na Mboza Lwandiko
Lipa Kodi ya Ardhi kwa wakati, uepuke kutozwa Tozo, Kutangazwa kwenye Vyombo vya Habari, Kupelekwa Mahakamani na Kufutiwa umiliki wa ardhi yako, kwani Sheria  ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 inaainisha gharama hizo kwa wasiozingatia ulipaji Kodi. kutozingatia kulipa Kodi ya pango la Ardhi kwa wakati, ambapo mmiliki asiyezingatia hilo kwanza; atatozwa Tozo na baadae Kupelekewa hati ya madai na kufikishwa Mahakamani kulingana na kifungu Na. 50 na hatimaye kufutiwa umiliki wa ardhi kulingana na Sheria hiyo hiyo katika kifungu Na. 49-51.
Akizungumza na Waandishi wa habari hivi karibuni wakati wa zoezi la kutoa notisi ya siku 14 kwa wadaiwa sugu wa Kodi ya Pango la Ardhi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Dkt. Yamungu Kayandabila amesisitiza kwa umma kuwa wadaiwa wote wa Pango la Ardhi wamekumbushwa na Serikali kwa muda mrefu, na hivyo ni wakati wao kuhakikisha wanalipa madeni yao yote ipaswavyo. Aliendelea kusema kuwa; kwa Mwaka wa fedha 2016/17 Wizara imepanga kukusanya Sh. bilioni 111.77 kutokana na Kodi ya Pango la Ardhi.  
Dkt. Kayandabila alisema kwakuwa Kodi ya Ardhi inatambulika bayana chini ya Sheria, kila mmiliki wa Ardhi hana budi kuzingatia hilo. Malipo ya pango la ardhi yanatozwa kwa wamiliki wa viwanja na mashamba yaliyopimwa na kumilikishwa kisheria. Pia mtu yeyote anayemiliki ardhi iliyopimwa kisheria iwe imeendelezwa au haijaendelezwa bado anapaswa kulipa kodi ya pango. Kila mmiliki anaongozwa na mkataba  wa kulipia kodi ya pango la ardhi kila mwaka tarehe 1 (Mosi) Julai, Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999 kifungu  cha 33 na kifungu kidogo cha 11 imetoa mwanya kwa walipa kodi kuendelea kulipa bila adhabu hadi tarehe 31 Desemba ya mwaka unaohusika. Baada ya hapo adhabu inatozwa. Mteja anapaswa kufanya malipo ya Kodi ya pango la Ardhi kwa kuwa ananufaika na matumizi ya ardhi hiyo.
Vile vile, Mkuu wa Kitengo cha Kodi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Bwn. Dennis Masami ameeleza kwa waandishi wa habari kuwa opereshini iliyoanza ya kutoa notisi ya siku 14 kwa wadaiwa  ni endelevu na kueleza kuwa hati za madai zaidi ya 5000 zimeshasambazwa jijini Dar es Salaam. Alitaja baadhi ya Kampuni ambazo zina madeni sugu ambazo zimepewa notisi ya siku 14 kulipa madeni ni pamoja na; Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) anayedaiwa Shilingi milioni 144 na Mwananchi Engineering wana deni la milioni 22. Kampuni nyingine ambazo zilipatiwa notisi ni; Mohamed Interprise waliokuwa na deni la milioni 73 na wameshalipa deni lote hivi karibuni na Lamada/Ilala – waliokuwa na deni la milioni 54, wamepunguza deni kwa kulipa milioni 25.            
Utaratibu wa ukadiriaji wa kodi ya ardhi hufanyika kwa kuzingatia ukubwa wa ardhi inayomilikiwa na thamani ya ardhi mahali ilipo (land value), vilevile kwa kuzingatia huduma muhimu zilipo (miundombinu) na Matumizi ya ardhi husika kama vile Biashara, viwanda, makazi, kilimo.
Aidha, Makadirio na malipo ya kodi ya ardhi Kwa wamiliki wa ardhi  yanafanyika katika maeneo mbalimbali. Dar es Salaam; malipo ya kodi hufanyika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi – Kivukoni, kwenye Kitengo cha Kodi na pia kwenye Ofisi za Ardhi za Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke. Katika Mikoa; makadirio hufanywa kwenye Ofisi za Ardhi zinazotambulika za Manispaa na Halmashauri za Miji na Wilayani kote nchini.
Aidha, Kumbukumbu za muhimu zinahitajika wakati malipo yanapofanyika, kwa wale ambao kumbukumbu zao za umiliki zilishaingizwa kwenye Kompyuta wanatakiwa wakumbuke namba ya kumbukumbu ya kulipia yenye tarakimu sita (Lot Id Number). Hatahivyo, wengine wote wanapaswa kufika katika maeneo yao ya kufanyia malipo na risiti/ stakabadhi ya mwisho ya malipo na hati au barua ya toleo (Original Letter of Offer).
Malipo ya kodi kwa toleo jipya la Kiwanja (Letter of Offer) yanapaswa kulipwa ndani ya muda wa siku 30 kuanzia tarehe ya toleo, vinginevyo itachukuliwa kwamba kiwanja kimekataliwa ambacho kilikuwa kimeshakabidhiwa kwa muhusika.
Katika Kampeni ya  uhamasishaji ulipaji Kodi ya Pango la Ardhi, katika eneo la  Mbagala – Dar es Salaam, zoezi lililofanywa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kushirikiana na Kitengo cha Kodi.  Afisa Sheria; Seif Mahiza, aliyekuwa akiongea na Wananchi wa Mbagala alisisitiza kuwa; “Mwananchi ataona mzigo wa kulipa pango lake la Kodi ya Ardhi pale tu atakapoacha kulipa kwa wakati na kuwa na malimbikizo, lakini Mwananchi akijitahidi kulipa kodi yake ya pango la Ardhi kila mwaka kwa wakati hataona mzigo katika kutimiza jukumu hilo”.
Malipo ya kodi ya Pango la Ardhi ni ya manufaa kwa Mmiliki ili kumhakikishia miliki salama na uhalali wa mali yake ambayo ina uwezo wa kuzalisha katika nyanja mbalimbali; mfano  katika kukopa, kuzalisha mazao, kukodisha n.k. Lakini pia Ardhi hiyo hiyo hutumika kunufaisha Taifa kwa ujumla kwa Maendeleo ya nchi nzima.
“Lipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa Maendeleo ya Taifa Letu”

0 comments: