Kapingaz Blog

Sunday, May 7, 2017

Rais Magufuli Awapa Tumaini Jipya Wafanya Biashara


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 06 Mei, 2017 alizindua Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuongoza Mkutano wa 10 wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baraza hili ni la tatu na mkutano huu ni wa kwanza kuongozwa na Mhe. Rais Magufuli tangu aingie madarakani ambapo tofauti na mikutano mingine, Mhe. Rais Magufuli aliendesha majadiliano ya pamoja ambapo wajumbe wa baraza na wawakilishi wengine kutoka sekta binafsi walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo na dukuduku, kisha kupatiwa majibu kutoka kwa Mawaziri, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Mhe. Rais.

Miongoni mwa yaliyojitokeza ni kuiomba Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango, sera na sheria mbalimbali za uwekezaji na biashara, kuendelea kuondoa vikwazo na urasimu ambao unachangia kupunguza ufanisi katika biashara na uwekezaji, kuongeza vivutio vya uwekezaji na kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi, utalii na viwanda.

Aidha, wawakilishi wa sekta binafsi waliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa inazozifanya kujenga miundombinu muhimu kwa uwekezajina biashara kama vile ujenzi wa reli, barabara, meli na ununuzi wa ndege, kukabiliana na rushwa, kusimamia mpango wa ujenzi wa viwanda, kujenga nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na kujenga uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali duniani.

Pamoja na majibu yaliyotolewa na Mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewaahidi wawakilishi wa sekta binafsi waliohudhuria mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha maoni yao yote yanafanyiwa kazi ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali zake na kusonga mbele kimaendeleo.

“Naomba niwahakikishie kuwa hisia zenu tumezipata, maoni yenu tutayazingatia na tutahakikisha tunayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kwa pamoja tufanye kazi ya kuijenga nchi yetu” alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Rais Magufuli aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Reginald Mengi kwa juhudi kubwa zinafanywa kuendeleza biashara na uwekezaji nchini na amewaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwathamini na kushirikiana na wawekezaji na wafanyabiashara kwa manufaa ya Taifa.

Mhe. Rais Magufuli alielezea kufurahishwa na maoni, mapendekezo na dukuduku alizozipata kutoka kwenye mkutano huo na amewakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa ikiwemo kuondoa usumbufu unaosababishwa na uwingi wa taasisi zinazomhudumia na kumtoza mfanyabiashara na mwekezaji, kuongeza vivutio, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi mbalimbali na kuishirikisha sekta binafsi katika mipango na utekelezaji wa miradi.

Kuhusu tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini Mhe. Rais Magufuli aliagiza kuanzia Jumatatu tarehe 08 Mei, 2017 taasisi zote zinazotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ziungane na Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutoa huduma kwa muda wote wa saa 24.

“Kama alivyosema Waziri Mkuu, tunataka kufanyia kazi maoni yenu mara moja, kuanzia Jumatatu nataka taasisi zote za pale bandarini zitoe huduma saa 24, haiwezekani bandarini kwetu mizigo ichukue siku 13 kuitoa bandarini wakati bandari za wenzetu majirani inatoka baada ya siku 3, tutashindana vipi?” alihoji Mhe. Rais Magufuli.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji wajirekebisha kwa kasoro ambazo baadhi yao wanazo ikiwemo ukwepaji wa kodi, kupandisha viwango vya bei kwa huduma wanazotoa Serikalini, kujihusisha na rushwa, kutaka faida kubwa isiyostahili bila kuwajali wananchi na kutochangamkia fursa za uwekezaji za ndani na nje ya nchi licha ya juhudi zake za kuwaleta viongozi na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.

“Nataka mjiulize amekuja Waziri Mkuu wa India, amekuja Rais wa Vietnam, amekuja Rais wa Uturuki, amekuja Rais wa Kongo (DRC), amekuja Rais wa Zambia, amekuja Rais wa Uganda, amekujaMfalme wa Morocco na wengine wengi, tumenufaikaje? Mbona wao wanakuja kuwekeza hapa nyie kwa nini hamuendi kwao?” alihoji Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

0 comments: