Kapingaz Blog

Wednesday, June 7, 2017

Askari wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia Wampongeza JPM


unnamed
Katibu wa Chama cha askari wastaafu waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia(TLC) Mzee Sylvester Lubala (katikati) akizungumza na waaandishi wa habari (hawapo pichani) juu kumuunga mkono  Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua katika vita ya madawa ya kulevya pamoja na kupiga vita uhujumu uchumi nchini, kulia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Mzee Rashid Bakari na kushoto ni Mjumbe wa chama hicho Mzee Damian Rashid.
Picha na Frank Shija – Maelezo
………………………….
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
CHAMA cha askari wastaafu waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia(TLC) wamempongeza na kumuunga mkono  Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua katika vita ya madawa ya kulevya pamoja na kupiga vita uhujumu uchumi nchini.
Hayo yamesemwa leo na Katibu wa chama hicho Mzee Sylvester Lubala wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuahirishwa kwa mkutano mkuu wa chama hicho uliokuwa umepangwa kufanyika Juni 9 hadi 10 jijini Dar es Salaam.
 “Chama cha Askari Wastaafu waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia tunapenda kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa hatua sahihi aliyochukua ya kupiga vita madawa ya kulevya ambayo yanawadhuru watoto na wajukuu wetu,” alisema Mzee Lubala.
Aidha katika hatua nyingine wazee hao wamemuomba Mhe. Rais Magufuli kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakuta hususani katika kupata huduma za afya kwani wamekuwa wakisumbuliwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha.
Pia wameishukuru serikali kwa kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuwasaidia kuwaarifu wajumbe wa chama hicho kote nchini kuhudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Taifa.
Awali mkutano mkuu wa chama hicho ulipangwa kufanyika Juni 9 hadi 10 lakini kutokana na mfungo wa Ramadhan wamelazimika kuahirisha hadi Julai 8 na utafanyika jijini Dar es Salaam.

0 comments: