Kapingaz Blog

Saturday, June 10, 2017

Wafamasia Watakiwa kuzingatia Maadili


FAM1
Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania Bi. Elizabeth Shekalaghe akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafamasia wanaotarajiwa kuanza kutoa huduma mara baada ya kuhitimu masomo yao na kula kiapo cha kuzingatia maadili ya taaluma hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
FAM2
Naibu Msajili wa Baraza hilo Bi. Zainabu Nyamungumi akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja kwa wafamasia wanaotarajiwa kuanza kutoa huduma baada ya kuhitimu masomo yao na kula kiapo,Leo Jijini Dar es Salaam.
FAM3
Afisa Usajili wa Baraza hilo Bw.Rashid Kiria akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo  hayo.
FAM4
Mmoja wa wafamasia hao akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika mapema leo Jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………………..
Frank   Mvungi-Maelezo
Wafamasia nchini wametakiwa kuzingatia maadili na weledi katika kutekeleza majukumu yao ili kuchochea azma ya Serikali  ya Awamu ya Tano kutoa huduma bora za afya kote nchini hali itakayochea maendeleo na ukuaji wa sekta hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Msajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth Shekalaghe wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafamasia waliohitimu masomo yao hivi karibuni katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi na kula kiapo cha kuzingatia maadili ya taaluma hiyo adhimu kwa mustakabali wa ukuaji wa sekta ya afya hapa nchini.
“Mafunzo haya yamehusisha takribani wafamasia 160 na yanalenga kuwakumbusha wajibu wao na umuhimu wa kuzingatia maadili na kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza wakati watakapokuwa wanatekeza majukumu yao kwa kuwa wapo watakafanya kazi katika Mikoa, Halmashauri na Hospitali katika maeneo mbalimbali “ alisisitiza Shekalaghe.
Akifafanua amesema kuwa  mafunzo hayo yameshafanyika katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Kaskazini,Mashariki na Kanda ya Ziwa dhamira ikiwa kuwajengea uwezo wafamasia wanaohitimu kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao mara baada ya kula kiapo.
Aliongeza kuwa jukumu la Baraza hilo ni kufuatilia mwenendo wa wafamasia ili kuhakikisha kuwa wanazingatia maadili ya taaluma hiyo na wamiliki wa maduka ya dawa kuhakikisha kuwa wanaajiri wafamasia wenye sifa na waliosajiliwa ili watoe huduma bora kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Baraza hilo Bi. Zainabu Nyamungumi akiwasilisha mada katika mafunzo hayo amesisitiza umuhimu wa wafamasia kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia taaluma hiyo katika maeneo watakayokuwa wanafanya kazi.
Pia aliwataka kutekeleza kwa vitendo yale waliyofundishwa katika mafunzo hayo ili kuchochea ukuaji wa taaluma hiyo.
Naye mdau wa Taaluma hiyo ambaye pia ni mwanataaluma Bw. Manase Kejo iliwataka wafamasia hao kujiamini na kujiajiri kwa kuwa taaluma waliyo nayo ni fursa inayoweza kuzalisha ajira.
“Ni muhimu mkatambua kuwa taaluma hii ni muhimu na jambo kubwa ni kutambua kuwa mnaweza kujiajiri,” Alisisitiza Kejo.
Mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na wafamasia takribani 450 na kufikia mwaka 2017 wamefikia 1600 hali inayoonyesha kuwa taaluma hiyo inaendelea kukua kwa kasi suala linalochagizwa na ongezeko la  vyuo vinavyotoa taaluma hiyo kikiwemo Chuo Kikuu cha Mtakatifu John Dodoma, Bugando na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi  Shirikishi Muhimbili

0 comments: