Kapingaz Blog

Tuesday, July 11, 2017

Kauli ya Mbowe Baada ya Halima Mdee Kuachiwa Kwa Dhamana

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amezungumzia sakata la kukamatwa kwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye aliachiwa jana kwa dhamana.

Mdee alishikiliwa na jeshi la polisi kwa siku tano kufuatia amri ya kukamatwa iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi baada ya kudaiwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais John Magufuli. Mdee alifikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kumkashfu Rais.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka mahakamani jana, Mbowe alisema kuwa Mdee alieleza kuhusu hisia zake na sio vinginevyo kuhusu agizo la Rais Magufuli kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaopata ujauzito hawataruhusiwa kuendelea na masomo.

“Sisi kama chama na kama viongozi, tunaamini kila Mtanzania awe kiongozi asiwe kiongozi, wa chama chochote na wa dini yoyote ana haki ya kueleza hisia zake.

"Mdee amesomewa mashtaka ambayo sitaki kuyazungumzia, lakini utamaduni huu mpya unaojengwa ndani ya taifa wa kuziba midomo watu wasiseme hisia zao, utajenga chuki katika jamii. Sisi kama chama cha kupigania haki tunaamini, kila mtu ana haki ya kueleza hisia zake.

“Halima ni mbunge, ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha). Kwahiyo ni kiongozi mwandamizi, sio tu wanatakiwa waseme anatakiwa akemee. Alipokuwa anazungumza kuhusu watoto kupata mimba alikuwa anazungumza kama mwanamke, Mbunge na Mwenyekiti wa Bawacha,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongeza kuwa chama chake kitaendelea na mjadala huo bila kujali hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yao.

0 comments: