Kapingaz Blog

Thursday, August 3, 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Latoa ripoti ya hali ya kisiasa nchini Burundi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema kuwa linasikitishwa na hali mbaya ya kisiasa nchini Burundi zikiwemo taarifa za ongezeko la idadi ya wakimbizi na taarifa za mateso, kupotea kwa watu na mauaji ya kinyama.

Katika ripoti hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limesema kuwa limekusudia kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na matukio hayo ndani na nje ya nchi hiyo kwakuwa wanatishia amani na usalama wa Burundi.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Balozi,  Amr Abdellatif Aboulatta wa Misri ambaye ndio mwenyekiti wa Baraza hilo, amesema kuwa baraza hilo linasikitishwa na hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea Burundi ambapo zaidi ya wakimbizi laki mbili wamekuwa wa ndani, huku watu raia milioni tatu wakiwa na mahitaji na zaidi ya raia laki nne wakitafuta ukimbizi katika nchi za jirani.

Aidha, Baraza hilo limeshukuru nchi zinazopokea wakimbizi kwa jitihada zao, mataifa ya kikanda kwa kuheshimu wajibu wao wa kimataifa hasa katika kujali hadhi za wakimbizi na kuhakikisha wanarejea waliokotoka kwa hiari yao kwa kuzingatia uamuzi wao na taarifa za usalama na utu wa binadamu.

Hata hivyo,  Baraza hilo limelaani vikali matamko ambayo yamekuwa yakihamasisha vurugu na chuki dhidi ya raia ikiwemo wito wa kulazimisha kuwapa ujauzito wanawake na wasichana na kuitaka Serikali na pande zote kusitisha mara moja vurugu na kulaani kauli zote za chuki.

0 comments: